HABARI MPYA

Friday, October 31, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Chama cha Mapinduzi kimepokea kwa furaha matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Msumbiji tarehe 15 Oktoba 2014. Chama Cha Mapinduzi kilikuwa kinafuatilia kwa karibu mchakato wote wa Uchaguzi huo hasa kwa sababu Tanzania na Msumbiji ni nchi zenye uhusiano wa damu.
Kilifuatilia kwa karibu kwa kuwa pia CCM na Chama cha FRELIMO ni vyama ndugu vyenye historia moja na ya pamoja ya Ukombozi Kusini mwa Afrika.
Historia hiyo ndiyo iliyomfanya Rais Mteule wa nchi hiyo Ndugu Filipe NYUSI mara baada ya kuteuliwa kwake na FRELIMO kugombea Urais, nchi ya kwanza kuitembelea kuwa Tanzania.
Ikumbukwe kwamba huyu si mgeni hapa Tanzania. Kama wanaharakati wengine wa ukombozi, Ndugu NYUSI aliishi Tanzania, anaongea vizuri Kiswahili na anaichukulia Tanzania ni nyumbani.
Kwa mnasaba huo, Chama Cha Mapinduzi na Watanzania kwa ujumla tuna kila sababu ya kushangilia ushindi walioupata ndugu zetu wa FRELIMO, kwani ushindi wao ni ushindi wetu.
Tunampongeza sana Rais Mteule Filipe NYUSI kwa kupeperusha vema bendera ya FRELIMO. Matokeo ya Uchaguzi yamedhihirisha imani kubwa waliyonayo wana-Msumbiji kwa FRELIMO na kwa Rais Mteule Filipe NYUSI.
Tuna imani kwamba chini ya uongozi imara wa Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, na Rais Mteule Filipe NYUSI, uhusiano kati ya vyama vyetu viwili utaimarika na kustawi.
Tunampongeza pia Rais Armando GUEBUZA kwa kuiongoza FRELIMO na Taifa lake vema na kukamilisha uongozi wake kwa mafanikio makubwa. Tunamtakia maisha tulivu ya kiongozi huyo mstaafu.
Anapoanza kipindi hiki cha uongozi wa Taifa lake, sisi wana-CCM tunamtakia Ndugu NYUSI afya njema, busara, maarifa na uongozi uliotukuka.
CCM itasimama pamoja na FRELIMO katika kuendeleza urithi ulioachwa na waasisi wa vyama vyetu Mwalimu Julius NYERERE na Ndugu Samora MACHEL.
Imetolewa na:-
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
ITIKADI NA UENEZI
31/10/2014

No comments:

Post a Comment